
Paul Magoiga
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
Wananchi wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara wamepokea kwa furaha hatua ya serikali ya kuanza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilitiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo, mradi ambao ulikuwa umekwama kwa miaka takribani 20.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mambokaleo, serikali imetenga shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza na Mara Online News juzi, mkazi wa wilaya ya Serengeti, Paul Magoiga alisema hatua hiyo imeonesha matumaini na mwanga kwa wana-Serengeti ambao waliibua wazo la ujenzi wa uwanja huo.
“Uwanja huu ulianza kuangaziwa na wananchi wa Serengeti kwa muda mrefu kwa ajili ya kuhudumia watalii wanaomiminika kwa wingi kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja kuangalia vivutio vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.
“Kutokana na serekali yetu kuona umuhimu wa kujenga uwanja huo, matarajio yetu ni kuona pato linalotokana na utalii linaongezeka kwa wana-Serengeti, wana-Mara na taifa kwa ujumla.
“Tunaishukuru serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuuona umuhimu wa kuanza ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa Serengeti, Mungu ambariki sana,” alisema Magoiga.
Kwa mujibu wa Magoiga, wananchi wa Serengeti wanaamini mradi wa ujenzi wa uwanja huo utakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwao na taifa kwa ujumla.
“Tunaomba serikali iharakishe mradi huu wa kimkakati kwani utakuwa na manufaa makubwa kwani utatosheleza mahitaji ya watalii wengi kutokana na juhudi za Rais Samia za kukuza utalii nchini kupitia filamu yake ya Royal Tour.
“Tunamwombea Rais wetu afya njema na nia ya serikali yake ipate kutimiza azima hii njema kwa taifa letu. Mungu ambariki Rais wetu na serikali yake katika utekelezaji wa mradi huu wa manufaa,” alisema Magoiga.
No comments:
Post a Comment