
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi.
Na Mwandishi Wetu, Serengeti
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, ameiagiza Idara ya Wanyamapori Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuanzisha kituo maalum cha kufuatilia na kudhibiti wanyamapori wanaovamia maeneo ya wananchi.
Kanali Mtambi ameelekeza uanzishaji wa kituo hicho ukamilike ndani ya muda wa wiki mbili kuanzia siku aliyotoa agizo hilo ili kuepusha madhara yanayosababishwa na Wanyama hao kwa wananchi katika vijiji vinavyopakana na maeneo ya uhifadhi.
“Ndani ya wiki mbili nataka kituo hicho kiwepo na mhakikishe mnawapa wananchi taarifa muhimu, kuwaelimisha jinsi ya kukitumia na kuwapa namba za simu zitakazokuwa zinapokewa wakati wowote watakapopiga kuomba msaada,” Kanali Mtambi aliagiza wakati akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Makundusi Aprili 17, 2025.
Awali, wakazi wa kijiji hicho walilalamika kwa kiongozi huyo wa mkoa wakisema kumekuwepo na ongezeko la matukio ya wanyamapori, hasa simba na tembo kuvamia maeneo yao na kusababisha madhara kwa mali zao, lakini pia kutishia usalama wa maisha yao.
“Mkuu wa Mkoa, hivi tunavyoongea kuna mwenzetu yupo hospitalini baada ya kushambuliwa na simba juzi, na haya matukio yamekuwa yakitokea mara kwa mara. Hivyo, tunaomba usaidizi wa serikali ili kumaliza tatizo hili,” alisema mkazi wa kijiji hicho, Lucas Kosuri.
Wanakijiji wengine, Mtuki Marwa na Owino Kagoro, walieleza kuwa mbali na kukujeruhi watu, wanyamapori wamekuwa wakivamia na kuharibu mashambani yao na kuua mifugo malishoni na mazizini.
Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, John Lendoyan, alipoulizwa alikiri kuwepo kwa matukio hayo.
“Ni kweli hapa kuna tatizo la wanyamapori, hasa simba na tembo kuvamia kijiji na kuharibu mali na kujeruhi watu,” alisema Lendoyan na kuahidi kushirikiana na wenzake kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa la kuanzisha kituo hicho.
No comments:
Post a Comment