
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephen Kiruswa (aliyeshikia vipaza sauti), akizungumza na wananchi mkoani Shinyanga jana katika eneo ilipotokea ajali ya wachimbaji wadogo wa madini kufukiwa mgodini.
---------------------------------------
Timu ya uokozi kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu iko mkoani Shinyanga kuongeza nguvu za kuwaokoa wachimbaji wadogo wa madini zaidi 20 waliofunikwa na kifusi katika Mgodi wa Dhahabu wa Nyandolwa.
Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, kama ulivyo mgodi mwingine wa Dhahabu wa North Mara, wilayani Tarime, mkoani Mara, unaendeshwa na kampuni ya kimataifa ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals,
Migodi hiyo miwili ya dhahabu nchini Tanzania katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ni chanzo kikubwa cha mapato ya serikali katika kuimarisha uchumi wake.
Jumatatu wiki hii katika mgodi wa Nyandolwa, wachimbaji wadogo 25 walifunikwa na kifusi kilichosababishwa na kuporomoka kwa udongo wakati wakiwa katika shughuli zao.
Jana, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stephen Kiruswa, alitembelea eneo la ajali na kuwataka wataalamu wa uokozi kuongeza kasi na kuhakikisha kwamba kazà hiyo inakamilika kwa ufanisi.
Hadi kufikia jana, wachimbaji wanne kati ya 25 waliofukiwa na kifusi walikuwa wameokolewa, ingawa baadaye mmoja wao aliripotiwa kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini.
Dkt Kiruswa aliahidi azima ya serikali kuendelea kushirikiana na vyombo vya uokozi katika tukio hilo la kusikitisha.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa familia, ndugu na jamaa husika akielezea kupokea kwa masikitiko makubwa tukio hilo.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya maafa yaliyotokea katika Mgodi wa Nyandolwa, kata ya Mwenge mkoani Shinyanga ambapo ndugu zetu 25 wanaofanya shughuli katika mgodi huo walifukiwa na kifusi.
“Nimeielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu na vyombo vya ulinzi na usalama kupeleka misaada ya haraka na kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuharakisha uokoaji.
“Tuendelee kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie pona ya haraka majeruhi, na pia awape subra na nguvu ndugu, jamaa na marafiki wa wale wote walioathiriwa na maafa haya,” alisema Rais Samia.
No comments:
Post a Comment