
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi (katikati), alipowasili katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuzindua mradi wa chanzo cha maji kwa ajili ya vijiji 11 wiki iliyopita. Kushoto ni Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Tulimpoki Mwakalukwa (kulia).
-------------------------------------------
Hatimaye ndoto ya kupata maji safi na salama kwa maelfu ya wananchi wa vijiji 11 vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara inakaribia kuwa halisi.
Hii ni kutokana na uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa chanzo cha maji kilichopo ndani ya mgodi huo, uliofanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, Agosti 21, mwaka huu.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 2.665 ni zao la mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) kutoka kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
Huo ni mfano bora wa jinsi sekta binafsi na serikali zinavyoweza kushirikiana kwa ufanisi kubadilisha maisha ya wananchi wa kawaida.
Kabla ya upanuzi huo, chanzo hicho cha maji kilikuwa kimesanifiwa kuhudumia vijiji vinne pekee, ambavyo ni Nyangoto, Matongo, Mjini Kati na Nyabichune, kwa wakazi 27,742.
Hata hivyo, kutokana na ongezeko la mahitaji, sasa chanzo hicho kinaboreshwa ili kiweza kupanua huduma hadi kwa wakazi 125,566 wa vijiji vingine vipatavyo saba - Kewanja, Genkuru, Nyamwaga, Nyakunguru, Kerende, Msege na Komarera. Hili si jambo dogo.
Kwa mujibu wa RUWASA, mradi huo umefikia asilimia 80 ya utekelezaji na utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 2.3 hadi lita zaidi ya milioni 10 kwa siku.
Kwa hiyo, wanawake na watoto hawatalazimika tena kutumia muda mrefu kutafuta maji; badala yake, wataweza kushiriki katika shughuli za kiuchumi, elimu na afya, hivyo kukuza ustawi wa familia zao na jamii kwa ujumla.
Tunapojadili maendeleo ya nchi yetu, hatuwezi kupuuza mchango wa huduma za msingi kama maji, afya na elimu. Maji safi ni msingi wa afya bora na maisha yenye heshima.
Kwa muktadha huo, pongezi si tu kwa kampuni ya Barrick kwa kuonesha mfano bora wa uwajibikaji kwa jamii, bali pia kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na ushirikiano wenye tija.
Aidha, hatuna budi kuipongeza RUWASA – hususan Mkoa wa Mara – kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maji kwa kiwango kinachotambuliwa kitaifa. Hakuna maendeleo pasipo usimamizi makini wa rasilimali, na RUWASA wamethibitisha kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano wa wazi.
Tunaamini kuwa mradi huo si wa mwisho. Tunatoa rai kwa wawekezaji wengine kufuata nyayo za Barrick – si kwa kushurutishwa, bali kwa kutambua kuwa ustawi wa jamii inayowazunguka ni sehemu ya mafanikio ya uwekezaji wao. Pale ambapo jamii inanufaika, ndipo panapokuwa na amani, mshikamano na uendelevu wa biashara.
Mwisho, Mara Online News tunawakumbusha wananchi wa vijiji husika kwamba miradi ya maendeleo inayotekelezwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara ni mali yao, hivyo watoe ushirikiano katika kuilinda na wahakikishe kuwa matokeo ya uwekezaji huo yanakuwa endelevu hadi kwa vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment