Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).
--------------------------------------------------
-----------------------------------------
Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili mkoani Mara kesho Julai 26, 2024 na kupokewa mapema asubuhi katika uwanja wa Shule ya Msingi Robanda wilayani Serengeti.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Musoma leo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi amesema maandalizi ya kupokea na kukimbiza Mwenge huo mkoani Mara yamekamilika kwa asilimia 100.
Mtambi amebainisha kuwa ukiwa katika mkoa wa Mara, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya sita na halmashauri tisa katika umbali wa kilomita zaidi ya 1,000.
Amesema Mwenge huo unatarajiwa kupita katika miradi ya maendeleo 72 yenye thamani ya shilingi bilioni 24.961 mkoani Mara, ambayo imetekelezwa kutokana na michango iliyotolewa na wananchi, halmashauri, Serikali Kuu na wahisani.
“Miradi itakayotembelewa ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, mazingira, ustawi wa Jamii, viwanda na biashara na shughuli za vijana,” amesema Mtambi.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2024 unahamasisha utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa serikali za mitaa chini ya kaulimbiu inayosema: “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi amewakaribisha viongozi, watendaji na wananchi wote kushiriki katika maadhimisho ya miaka 60 ya Mwenge wa Mwitongo yatakayofanyika nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wilayani Butiama Agosti 1, 2024.
Mwenge wa Mwitongo ni wa kabila la Wazanaki ambao upo nyumbani kwa Baba wa Taifa, na unawashwa kila mwaka wakati Mbio za Mwenge wa Uhuru zikiwa katika mkoa wa Mara, tangu mbio hizo zilipoanzishwa mwaka 1964.
“Mwaka huu ni mwaka maalum kwa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo unaadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 60 ya Muungano wa Tanzania na miaka 60 ya Mbio za Mwenge wa Uhuru,” amesema Mtambi.
Mtambi amewashukuru wananchi wa mkoani Mara ambao wamechangia kwa hali na mali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan itakayotembelewa na Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024.
Ametumia nafasi hiyo pia kuwalika wananchi wote kushiriki mbio, mapokezi, mikesha na shamrashamra za Mwenge wa Uhuru kipindi chote utakapokuwa mkoani Mara.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
- >>Mwenge wa Uhuru 2024 waanza mbio zake mkoani Mara
- >>Mwenyekiti CCM Mara:Tumejipanga vizuri kuupokea Mwenge wa Uhuru kesho
- >>TIC watembelea kahawa ya Tarime inayotamba soko la dunia
- >>Nyambari akutana na Spika wa Bunge la Tanzania jijini New Delhi
- >>Mwenyekiti UWT CCM Mara ahamasisha wanawake wilayani Tarime kugombea uongozi, wavuna wanachama wapya
- >>Maswi, Ridhiwan wang’ara teuzi za Rais Samia, Nape na Makamba wavuliwa uwaziri, Mashinji na Afraha wahamishwa Serengeti
No comments:
Post a Comment