
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
-----------------------------------------------
Na Mwandishi Wetu
-----------------------------
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amesema chama hicho kimejipanga vizuri kwa ajili ya kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kuwasili mkoani humo kesho Ijumaa.
“Tumejipanga vizuri na tunaukaribisha sana Mwenge wa Uhuru katika mkoa wetu wa Mara,” Chandi ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu kutoka wilayani Serengeti leo Julai 25, 2024.
Kiongozi huyo wa mkoa ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kuupokea na kuukimbiza Mwenge huo kwa vigelegele na vifijo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuwasili na kupokewa mkoani humo kesho asubuhi katika uwanja wa Shule ya Msingi Robanda wilayani Serengeti.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Musoma mapema leo, Mtambi amesema maandalizi ya kupokea na kukimbiza Mwenge huo mkoani Mara yamekamilika kwa asilimia 100.
Amebainisha kuwa ukiwa katika mkoa wa Mara, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya sita na halmashauri tisa katika umbali wa kilomita zaidi ya 1,000.
Amesema Mwenge huo unatarajiwa kupita katika miradi ya maendeleo 72 yenye thamani ya shilingi bilioni 24.961 mkoani Mara, ambayo imetekelezwa kutokana na michango iliyotolewa na wananchi, halmashauri, Serikali Kuu na wahisani.
“Miradi itakayotembelewa ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, mazingira, ustawi wa Jamii, viwanda na biashara na shughuli za vijana,” amesema Mtambi.
Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2024 unahamasisha utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa serikali za mitaa chini ya kaulimbiu inayosema: “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu”.
No comments:
Post a Comment