NEWS

Friday, 26 July 2024

Mwenge wa Uhuru 2024 waanza mbio zake mkoani Mara



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi (mwenye miwani) akishiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mara baada ya kuwasili wilaya ya Serengeti mkoani Mara ukitokea mkoa wa Arusha mapema leo Julai 26, 2024 asubuhi. Mwenye shati la madoa ya kijani kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.
-------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
------------------------------------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi ameshiriki mapokezi ya mbio za Mwenge wa Uhuru ambao  umewasili mkoani humo kutokea mkoa wa Arusha.

Mapokezi hayo yamefanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Robanda wilayani Serengeti mapema leo Julai 26, 2024 asubuhi, mara baada ya Mwenge huo kuwasili ukitokea mkoani Arusha.

RC Mtambi akizungumza wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Serengeti.
--------------------------------------------

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mkoa, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya sita na halmashauri tisa katika umbali wa kilomita zaidi ya 1,000 mkoani Mara.

Amefafanua kuwa mwenge huo utapita katika miradi ya maendeleo 72 yenye thamani ya shilingi bilioni 24.961, ambayo imetekelezwa kutokana na michango iliyotolewa na wananchi, halmashauri, Serikali Kuu na wahisani.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya akikabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marko baada ya kuupokea mapema leo asubuhi ukitokea mkoani Arusha.
-----------------------------------------------

Mbio za Mwenge wa Uhuru zikiwasili mkoani Mara katika wilaya ya Serengeti mapema leo asubuhi ukitokea mkoani Arusha.
------------------------------------------------

“Miradi itakayotembelewa ipo katika sekta za elimu, kilimo, ujenzi, maji, afya, mifugo, mazingira, ustawi wa Jamii, viwanda na biashara na shughuli za vijana,” amesema RC Mtambi.

Katika juhudi za utunzaji wa mazingira, RC Mtambi amesema miti zaidi ya 15,000 imepandwa mkoani Mara katika kipindi hiki cha mbio za Mwenge wa Uhuru.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2024, Godfrey Mnzava akikagua bweni la wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Robanda Mchanganyiko wilayani Serengeti.
----------------------------------------------

Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2024 unahamasisha utunzaji wa mazingira na uchaguzi wa serikali za mitaa chini ya kaulimbiu inayosema: “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu.”
Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages