NEWS

Tuesday, 23 July 2024

TIC watembelea kahawa ya Tarime inayotamba soko la dunia



Wataalamu kutoka TIC Kanda ya Ziwa wakioneshwa sampuli ya kahawa iliyochakatwa  mjini Tarime jana.
------------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
------------------------------------

Timu ya wataalamu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kanda ya Ziwa imetembelea kiwanda cha kuchakata kahawa ikiwemo aina ya Arabica inayolimwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Katika ziara hiyo ya jana Julai 22, 2024, wataalamu hao wakiongozwa na Meneja Uhamasishaji, Felix John, pamoja na mambo mengine walipata fursa ya kujionea kahawa inayochakatwa katika kiwanda kinachomilikiwa na Chama Kikuu Cha Ushirika wa Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd).

Mbali na kuzungumzia kahawa aina ya Arabica inayotamba kwa ubora katika soko la dunia, Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye alieleza namna ushirika huo ulivyojikita kwenye biashara ya kahawa na shughuli nyingine za kilimo.


Meneja Mkuu wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye (kulia mbele) akiongoza wataalamu wa TIC kiwandani hapo.
---------------------------------------------------

“Msingi wa chama chetu ni kahawa kama shughuli mama, lakini pia tunasambaza mbolea na pembejeo za kilimo kwa wakulima hapa mkoani Mara.

“Zamani kahawa ilikuwa inauzwa kienyeji kwenye masoko ya minada. Baada ya kupata kiwanda na kupewa mkopo na serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) tumenunua mitambo ya kisasa.

“Kwa sasa kazi inafanyika kwa urahisi na ufanisi, tunauza kahawa moja kwa moja kwenye masoko yaliyopo Canada, Uingereza, Marekani na mashariki ya kati kama Misri,” alisema GM Gisiboye.

Aidha, wataalamu hao kutoka TIC pia walitembelea mgodi wenye mtambo wa kuchenjua dhahabu wa Matongo na Kampuni ya Northern Highlands Coffee ya mjini Tarime.



Read Also Section

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages