NEWS

Monday, 18 November 2024

Maguge sasa rasmi Askofu mpya wa KKKT Dayosisi ya Mkoani Mara



Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt Alex Malasusa akizungumza katika ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu John Maguge (aliyekaa) wa KKKT Dayosisi ya Mkoani Mara mjini Musoma jana Novemba 17, 2024.
----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof Paramagamba Kabudi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kwa Askofu Mteule John Maguge wa KKKT Dayosisi Mkoani Mara.

Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa Kuu la Nyasho, Musoma jana. Maguge sasa ni Askofu wa Nne wa KKKT Dayosisi Mkoani Mara. Ameingizwa kazini mbele ya Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt Alex Malasusa, mtangulizi wake, Askofu Michael Adam akisaidiana na Askofu Dkt Benson Bagonza na Askofu Nicholaus.

Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Kabudi alisema maombi yaliyotolewa na Askofu Maguge kwa serikali yatafanyiwa kazi.

Maombi hayo ni pamoja na ukamilishaji wa Uwanja wa Ndege wa Musoma, ujenzi wa barabara za lami Tarime–Mugumu na Butiama–Nyamuswa.

“Muwe na amani mambo yataenda vizuri,” Prof Kabudi alisisitiza.

Waziri huyo wa Katiba alisema maombi ya viongozi wa dini ni chachu ya kudumisha amani nchini.

Waziri Kabudi akisalimiana na maaskofu alipomwakilisha Rais Samia kwenye ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Maguge.
---------------------------------------

Kwa upande wake Askofu Malasusa alimtaka Askofu Maguge kutambua kuwa Bwana Yesu ndiye aliyemuita katika nafasi hiyo, hivyo anapaswa kutenda mapenzi yake katika kazi ya uaskofu aliyoitwa na Mungu.

Aidha, alisema Wakristo wanapaswa pia kukumbuka kuwa ni nani aliyewapa talanta walizonazo na hivyo ni vema watamani kumjua zaidi Mungu ili kuweza kuyatimiza mapenzi yake katika nafasi mbalimbali walizonazo.

Katika mahubiri hayo, Askofu Malasusa pia aliwataka wachungaji kukumbuka wajibu wao kuwa ni kukusanya na kulisha kundi la Mungu, na ili wafanye hivyo wanapaswa kuendelea kukaa ndani ya Mungu na kumpenda zaidi.
Read Also Section Example

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages