
Mwenyekiti ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali (Mst) George Marwa Waitara (kushoto), akitoa maelekezo kwa menejimenti ya shirika hilo kuhusu ujenzi wa daraja la Mto Kogatende katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wiki iliyopita.
--------------------------------------
Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imeiagiza menejimenti ya shirika hilo kuhakikisha kuwa ujenzi wa daraja la Mto Kogatende unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili kuruhusu shughuli za uhifadhi na utalii kuendelea.
Mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali (Mst) George Marwa Waitara, alitoa maagizo hayo wiki iliyopita, wakati walipotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kujionea daraja hilo ambalo kwa sasa halipitiki kutokana na uharibifu mkubwa uliosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2020 na 2024.
“Ujenzi wa daraja ufanyike kwa wakati bila kikwazo chochote kwani ni muhimu sana kwa ustawi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kiutalii na kiuhifadhi. Tunahitaji miundombinu imara katika hifadhi zetu ili shughuli za uhifadhi na utalii ziweze kufanyika vizuri.
“Ujenzi wa daraja hili ni suluhisho la kudumu na menejimenti ihakikishe mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa ubora ili liweze kupitika kwa kipindi chote cha mwaka,” Waitara alisema.
Naye, CPA Khadija Ramadhani, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA alisema “Kuna haja ya kuwa na daraja la juu kwa sababu hisitoria inaonesha kwamba daraja hili ambalo awali lilikuwa mita tano limeendelea kupanuka hadi kufikia mita 126.
“Gharama za upanuzi zimekuwa zikiongezeka kila wakati, hivyo kuna haja ya kujenga daraja la kudumu ili kuepuka gharama za matengezo ya mara kwa mara kwa menejimenti,” alisema.
Akieleza historia ya daraja hilo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Stephano Msumi, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, alisema kwamba awali daraja hilo lilikuwa la boksi (vented drift) ambalo lilikuwa likitumika wakati wa kiangazi tu kutokana na kuwa la chini.
“Daraja hili lilikuwa la boksi na lilikuwa chini na hivyo kupitika wakati wa kiangazi tu. Hata hivyo, limeendelea kuharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na mvua zilizonyesha mwaka 2020 na 2024 ambapo kulikuwa na mvua kubwa sana,” alisema Kamishna Msumi.

Mpaka sasa, tayari uchambuzi wa taarifa za awali umeshafanyika ili kubainisha kina cha maji katika Mto Kogatende, hali ya udongo katika eneo la ujenzi wa daraja na historia ya ukubwa wa mafuriko katika mto huo kwa miaka 30 iliyopita, ili kubainisha kimo cha daraja na kuwezesha usanifu wa michoro utakaokidhi viwango.
“Kazi inayoendelea hivi sasa ni ukamilishaji wa usanifu wa kina na kuandaa michoro na nyaraka za zabuni, ili kuanza taratibu za manunuzi ya mkandarasi,” Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Nuhu Daniel, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mendeleo ya Hifadhi alifafanua,
“Tunaendelea kukamilisha usanifu wa kina kwa ajili ya maandalizi ya nyaraka za zabuni ya manunuzi ya mkandarasi yaweze kufanyika ili kuwezesha ujenzi kuanza. Ujenzi wa daraja hili unakwenda kubadilisha kabisa uendeshaji wa utalii upande wa Kaskazini ambapo waendesha utalii wataweza kutumia upande wa pili wa mto katika eneo la Lamai kiutalii, hasa msimu wa uvukaji wa nyumbu katika Mto Mara.
Mradi wa ujenzi wa daraja la Kogatende lenye urefu wa mita 100, unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na utagharimu Euro milioni 2.2 sawa na shilingi za Tanzania takriban bilioni 6.3, na unatarajiwa kuanza Novemba, 2025.
Mradi huo ni sehemu ya mwendelezo wa ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani.
Bodi pia ilitembelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambayo ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Banagi - Lobo - Lango la Kleins yenye urefu wa kilomita 72, barabara ya Golini - Naabi - Seronera yenye urefu wa kilomita 68, ujenzi wa Uwanja wa Golf “Serengeti National Park Golf Course” inayotekelezwa na kampuni tanzu ya TANAPA “TANAPA Investment Limited (TIL)” na ujenzi wa lango la Kleins unaotekelezwa na kampuni ya Stance Technic and Civil Engineers Limited.
Bodi hiyo ilihitimisha kikao chake cha 209 wiki iliyopita, ambacho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya TANAPA, chini ya Mwenyekiti wake, Jenerali (Mst) Waitara.
Kikao hicho kilitanguliwa na vikao vya Kamati ya Ukaguzi na Utawala Bora inayoongozwa na CPA Hadija Mohamed Ramadhani, Kamati ya Himasheria na Usimamizi wa Hifadhi inayoongozwa na Dkt Robert Fyumagwa na Kamati ya Utalii na Huduma za Shirika inayoongozwa na Dkt Rhimo Nyansaho.
UNAWEZA PIA KUSOMA:
»Serengeti: Mwenyekiti UVCCM Mara aunga mkono Serikali kufanikisha upatikanaji wa lishe mashuleni
»Kazi na Utu: Urithi wa JPM na mustakabali wa taifa letu
»MAKALA MAALUMU:Nyambari Nyangwine awa lulu mkoani Mara, aombwa kujitokeza kuomba ubunge wakati ukifika
»Taasisi ya Mwanzo Mpya yafuturisha Waislamu msikiti wa Masjid Sunni Tarime
No comments:
Post a Comment