
Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Emmanuel Nchimbi akipunga mkono kusalimia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara mjini Musoma jana Aprili 23, 2025. Kushoto ni Mwenyekiti wa Mkoa wa chama hicho, Patrick Chandi na wa tatu kutoka kushoto ni MNEC Christopher Gachuma.
-------------------------------------
Na Mwandishi Wetu, Musoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Emmanuel Nchimbi, jana Aprili 23, 2025 alikagua ujenzi wa ukumbi mpya wa kisasa wa chama hicho mkoani Mara ambao umefikia hatua za mwisho kukamilika.
Dkt Nchimbi yuko mkoani Mara kwa ziara ya siku tano iliyoanza Jumanne iliyopita kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Ukumbi mpya wa CCM mkoani Mara utakuwa na uwezo wa kutumiwa na watu 2,000 hadi 2,500 kwa wakati mmoja.
Jana Dkt Nchimbi, pamoja na mambo mengine, alikutana na idadi kubwa ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara kuzungumzia masuala mbalimbali ya chama hicho tawala.

Mapema kabla ya kikao hicho na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara, Balozi Dkt Nchimbi alitembelea miradi miwili ya ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mjini Musoma.
Katika ziara yake, Dkt Nchimbi atatembelea wilaya zote za mkoa wa Mara -- Bunda, Butiama, Rorya, Musoma, Tarime na Serengeti -- na kuzungumza na wana-CCM kujiweka tayari kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment